Ili kufifiliza suala hilo na kujaribu kuonesha kuwa hajasalimu amri, Trump ameongeza vita vyake vya kiuchumi na China kwa kupandisha ushuru wa bidhaa za China kwa asilimia 125 sambamba na tangazo lake la kusitisha utekelezaji wa nyongeza ya ushuru kwa bidhaa za nchi nyinginezo kwa muda wa siku 90.
Juzi Jumatano na ikiwa ni wiki moja tu baada ya kuzidisha vita vya kibiashara na ushuru dhidi ya nchi zote duniani, hali ya kiuchumi ndani ya Marekani imeporomoka vibaya na kumlazimisha Trump atangaze kusimamisha utekelezaji wa siasa hizo mbovu kwa muda wa siku 90. Hapo hapo na katika kuendeleza siasa zake zilezile za majivuno, Trump amejigamba kwa kusema: "Kutokana na China kutoheshimu masoko ya dunia, nimeamua kuongeza ushuru wa bidhaa za China zinazoingia Marekani kwa asilimia 125."
Tangazo hilo la Trump la kusimamisha utekelezaji wa sera zake za ushuru kwa muda wa siku 90 halizijumishi nchi za Canada na Mexico. Ikulu ya White House imethibitisha habari hiyo na kusema kuwa bidhaa za nchi hizo zitaendelea kutozwa ushuru mkubwa.
Uamuzi wa Trump wa kusimamisha sera zake hizo kwa muda wa siku 90 umenyanyua masoko ya Marekani licha ya kuziongezea ushuru bidhaa zinazotoka China. Kwa mfano, baada ya tangazo hilo la Trump zaidi ya dola trilioni 4 zimeingia kwenye soko la hisa la Marekani. Baada ya uamuzi huo wa Trump, thamani za hisa za makampuni kama Nvidia, Apple, Tesla na Microsoft zimepanda kwa asilimia kati ya 7.8 hadi 13.
Siasa za kidikteta za Trump za kupandisha ushuru wa bidhaa zinazoingia Marekani umezusha mgogoro mpya wa kiuchumi duniani na hasa kwa mashirika ya ndani ya Marekani kwani nchi mbalimbali ulimwenguni zimeamua kukabiliana kivitendo na sera hizo za kiistikbari za Trump. Katika kipindi kifupi tu cha kuingia madarakani Trump, ameyasababishia hasara kubwa masoko ya fedha ya Marekani na nje yake. Hasara hiyo inakadiriwa kupindukia dola trilioni 9 na nusu.
Trump amelazimika kusalimu amri na kulegeza kamba ingawa kwa ujanja wa kuzibakisha nchi kama China kwenye vita vyake vya kiuchumi baada ya kuona dunia nzima imesimama dhidi yake. Friedrich Merz, mgombea wa ukansela wa Ujerumani amesema kwamba, kulazimika Trump kusimamisha nyongeza ya ushuru kwa muda wa siku 90 ni ishara kwamba mshikamano uliooneshwa na nchi za Ulaya wa kukabiliana kivitendo na Trump umezaa matunda. Ametaka kuweko biashara isiyo na ushuru kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya. Bila ya shaka China nayo kamwe haitokaa kimya na tayari imepandisha ushuru kwa bidhaa zote za Marekani zinazoingia nchini humo. Beijing imetangaza kwamba itaendelea na vita hivyo hadi mwisho. China inategemea soko lake kubwa la bilioni ya watu kuipigisha magoti Marekani. Kuanzia jana Alkhamisi, China imesema imeongeza ushuru wa bidhaa za Marekani zinazoingia nchini humo kwa asilimia 84 hatua ambayo bila ya shaka ni pigo jingine kwa siasa za kibeberu na kidikteta za Trump na serikali yake huko Marekiani.
Wachambuzi wa mambo wanatabiri kuwa, hatua itakayofuatia ya Trump ni kutangaza kuwa nchi yoyote itakayoshirikiana na China katika vita vya kibiashara alivyovianzisha, itahesabiwa kuwa ni adui wa Marekani na itaongezewa ushuru kama China. Vile vile amedai kuwa nchi yoyote inayolipiza kisasi kwa kuziongezea ushuru bidhaa za Marekani, itakuwa imetangaza vita na Washington.
Licha ya matamshi ya Trump na madai yake kuhusu athari chanya za ushuru mpya kwa Marekani, lakini vita vya ushuru vya Trump vitazidisha mdororo wa uchumi wa Marekani, vitashadidisha mgogoro wa biashara ya kimataifa, vitashtadisha mfumuko wa bei na kleta uharibifu wa minyororo ya kimataifa ya ugawaji na usambazaji wa bidhaa. Vilevile vitapunguza kasi ya ukuaji wa uchumi, vitaongeza gharama za maisha na kuibua vita vya dunia vya kibiashara kati ya mataifa makubwa ya kiuchumi. Tayari hivi sasa kumeshazuka vita vikubwa vya kiuchumi na ushuru kati ya Marekani na China ikiwa ni kiashiria cha wazi za hatari ya kuzuka vita hivyo vikubwa vya kiuchumo kote ulimwenguni.
342/
Your Comment